Vijana wa Korea walioshiriki kambi ya
kimataifa ya vijana wakitumbuiza wakati wa ufungaji wa kambi hiyo jana Chuo
Kikuu cha Dar es Salaam.
Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Dkt.
Fenella E. Mukangara akipokea tuzo kutoka kwa Katibu Mkuu wa International Youth
Fellowship Bw. Lee Hunmok jana wakati wa ufungaji wa kambi ya kimataifa ya
vijana Jijini Dar es Salaam. Tuzo hiyo ilitolewa kwa Wizara kama ishara ya
kutambua mchango wake katika kuhakikisha kuwa maendeleo ya vijana yanastawi
kikamilifu.
Na Concilia Niyibitanga
WHVUM
Tarehe 8/8/2012
Maendeleo ya vijana ndiyo msingi wa maendeleo
ya taifa letu, na ni muhimu vijana wakatambua hilo kwa kutimiza wajibu wao kwa
jamii inayowazunguka.
Hayo yalisemwa jana na Waziri wa Habari, Vijana,
Utamaduni na Michezo, Dkt. Fenella E. Mukangara wakati akifunga kambi ya kimataifa
ya vijana Chuo Kikuu cha Dar es Salaam iliyokaa kwa muda wa siku saba kwa lengo
la kuzungumzia mustakabali wa maendeleo ya vijana hususan
kuwajengea vijana fikra chanya kwa ajili ya kujiletea maendeleo.
Dkt. Mukangara alisema kuwa vijana wanatakiwa kuwa
na moyo wa kujituma, kujitolea na kufanya kazi kwa bidii ili kukabiliana
na changamoto zinazowakabili katika maisha yao ya ujana.
‘Fanyeni kazi kwa bidii, kwa kujitolea, kwa
kuzingatia muda na kujitegemea ili kutimiza ndoto zenu za kujiletea maendeleo
ya kiuchumi na kiafya’. Alisema Dkt. Mukangara
Aidha, amewaasa vijana kuachana na fikra za
kulalamika, kudai haki bila wajibu na kunyosheana vidole na badala yake kijana
mwenyewe ajiulize amefanya nini kutatua kero inayomzunguka.
Vijana kataeni vitendo vya uchochezi, chuki na
kejeli kwa viongozi kwani kufanya hivyo kunaweza kuwaingiza katika misuguano
isiyo na tija na mkumbuke kuwa maendeleo ya vijana hayawezi kushamiri na
kustawi pasipo na amani, lindeni amani kwa nguvu zenu zote na kusimamia sheria
wakati wote’ Alisema Dkt. Mukangara.
Alisema kuwa Serikali inatambua umuhimu wa
vijana na kupitia Wizara yake imeweka mipango ambayo inatoa vipaumbele
kwa maendeleo ya vijana.
Naye Katibu Mkuu wa International Youth Fellowship
(IYF), Bw.Lee Hunmok aliwataka vijana kuwatumikia wenzao na kuwa mabalozi kwa
vijana ambao hawakupata fursa ya kuingia kambini.
Bw. Vitus Faustin Mzale ni kijana aliyeshiriki kambi
hiyo kutoka mkoani Kagera alisema kuwa ameweza kujifunza mambo mbalimbali
kambini hapo na amewataka waandaaji kushirikiana na Serikali ili kuwapa vijana
mafunzo ya ujasiriamali ili waweze kujikwamua kiuchumi.
Kwa upande wake Bi Mariza Vargas kijana kutoka
Peru alisema kuwa amefungua moyo wake kwa ajili ya kujitolea na ameweza
kujua namna ya kufanikisha malengo yake ya kujiletea maendeleo kama
kijana.
Kambi hiyo ya kimataifa iliyoandaliwa na International
Youth Fellowship ilishirikisha nchi mbalimbali ikiwemo Tanzania, Kenya, Korea,
Malawi, Peru na China.
_______________________________________
Media Contacts:
For more information, comments, please contact:
E-mail: thpi2009@gmail.com
No comments:
Post a Comment