Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha kupitia hospitali yake
ya AICC kitaendesha kampeni ya kupima kisukari bure kwa wakazi wa Arusha ili
kusaidia wananchi kutambua kama wana ugonjwa wa kisukari au wapo katika hatari
ya kuugua ugonjwa huo.
Kampeni hiyo itafanyika
kesho (terehe 26-07-2012) katika hopitali ya AICC iliyopo jijini Arusha ambapo
madaktari wa hospitali ya AICC kwa kushirikiana na Madaktari wanaohudhuria mkutano wa
Shirikisho la Madaktari wa Kimataifa pamoja na madaktari kutoka Chama cha
Ugonjwa wa Kisukari Tanzania wataendesha zoezi la upimaji huo.
Mkurugenzi Mwendeshaji wa
AICC, Bwana Elishilia Kaaya, amesema kuwa mbali na kupima kisukari, madaktari
hao pia watatoa ushauri wa namna bora ya kuishi na jinsi ya kuzuia madhara ya kisukari
kwa wale watakao kuwa wamekutwa na ugonjwa huo.
“Hospitali ya AICC
inatambua umuhimu wa afya za wakazi wa Arusha na Watanzania kwa ujumla na ndio
maana tumeona ni vema kufanya kampeni hii ya kupima kisukari. Napenda kutumia
fursa hii kuwaalika wakazi
wote wa Arusha na vitongoji vyake kufika kwa wingi kwani mbali na
kupima pia itatolewa elimu na ushauri kutoka kwa wataalamu hao.” alieleza
Kaaya.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mwendeshaji, upimaji huo
utaenda sambamba na mkutano wa kwanza wa Shirikisho la Madaktari wa Kisukari wa
Kimataifa ambao kwa mara ya kwanza unafanyika hapa nchini. Mkutano huo
utafanyika katika kituo cha AICC ambapo madaktari wanaohudhuria mkutano huo na
wale kutoka Chama cha Ugonjwa wa Kisukari Tanzania watatoa huduma ya upimaji
katika zoezi hilo.
“Tunaamini baada ya
kampeni hii wananchi watakuwa wamepata ufahamu juu ya hali ya afya zao na
kutumia vema ushauri wa madaktari kwa ajili ya kujikinga na kuzua athari za
ugonjwa huo”, alielezea Kaaya.
Mbali na kuendesha
kampeni hii, hospitali ya AICC imeanzisha kitengo maalumu cha kisukari ambapo
kila wiki madaktari hutoa huduma za matibabu na ushauri kwa wagonjwa wa
kisukri.
Ugonjwa wa kisukari
umekuwa ukiongezeka kwa kasi duniani ambapo taarifa za Shirika la Afrya Duniani
(WHO) zinaonesha kuwa hadi kufikia mwaka 2011 watu milioni 366 walikuwa
wanaugua ugonjwa wa kisukari na mwaka 2030 idadi inakadiriwa kufika milioni
552. Barani Afrika watu milioni 14 na nusu wanaugua ugonjwa huo huku idadi
ikitarajiwa kufika milioni 28 mwaka 2030 ikiwa ni ongezeko la 90%.
No comments:
Post a Comment