Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa
Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete amesema kuwa ni jambo lisilokubalika kwa mwanamke
kupoteza maisha wakati akijifungua kwa sababu uja uzito siyo ugonjwa.
Aidha, Dkt. Kikwete amesema kuwa pamoja na juhudi
kubwa zinazofanywa na Serikali katika kupunguza vifo vya akinamama wakati wa
uzazi na mipango mingine ya uzazi bora, bado tatizo linabakia kubwa na
zinahitajika juhudi zaidi ili kuondokana na tatizo la vifo wakati wa uzazi.
Dkt. Kikwete ameyasema hayo leo, Alhamisi, Julai 19,
2012, wakati alipokutana na kuzungumza na Mtendaji Mkuu wa shirika la kimataifa
lisilokuwa la kiserikali la Pathfinder International, Dkt. Purnima Mane, Ikulu,
Dar es Salaam.
Dkt. Kikwete amesema kuwa ni jambo lisilokubalika
kabisa kwa mwanamke kupoteza maisha wakati akijifungua.
“Uzazi siyo ugonjwa na kwa hakika ni
jambo lisilokubalika kwa mwanamke kupoteza maisha wakati akijaribu kutoa maisha
kwa binadamu mwingine. Hili ni jambo ambalo Serikali itaendelea kupambana nalo
hadi kulifikisha mahali pazuri zaidi.”
Dkt. Kikwete amesema kuwa ni kweli kuwa Serikali
yake imekuwa inafanya juhudi kubwa katika eneo hili lakini bado tatizo ni kubwa
na zinahitaji jitihada za ziada.
“Tumefanya jitihada kubwa na kupata
mafanikio ya kujivunia lakini bado kazi ni kubwa.”
Takwimu za sasa zinaonyesha kuwa akinamama 578 kati
ya 100,000 hupoteza maisha wakati wa uzazi, idadi ambayo imeshuka kutoka miaka
minne iliyopita wakati takwimu zilionyesha kuwa akinamama 790 kati ya laki moja
walikuwa wanapoteza maisha wakati wa kujifungua.
Miongoni mwa maamuzi ambayo Serikali imechukua
kukabiliana na tatizo hilo ni pamoja uamuzi wa kupunguza umbali wa kufikia
huduma za afya kwa kujenga zahanati kila kijiji na kituo cha afya kila kata na
hivyo kuhakikisha kuwa huduma hizo zinapatikana katika umbali usiozidi kilomita
tano.
Serikali pia imeamua kuwa kila zahanati ama kituo
cha afya lazima kiwe na huduma za kuhudumia wazazi na waja wazito.
Serikali pia imechukua hatua za kukabiliana na
ugonjwa wa ukimwi ambao ni moja ya chimbuko kubwa la vifo vya akinamama waja
wazito.
Dkt. Mane ambaye anatembelea Tanzania kwa mara ya
kwanza amemsifu Rais Dkt. Jakaya Kikwete kwa uongozi wake katika masuala ya
afya na masuala mengine.
“Uongozi wako katika suala hili ni jambo
linalojulikana duniani pote. Tunakushukuru sana kwa sababu wewe ni bingwa wetu
na msemaji wetu mkubwa katika mapambano ya usalama wa akinamama waja wazito.”
Pathfinder International ni shirika la kimataifa
lisilokuwa la kiserikali ambalo malengo yake makuu ni kushughulikia afya za
akinamama na kuboresha uzazi. Katika Tanzania, Pathfinder International
linaendesha miradi tisa kwa sasa katika maeneo ya UKIMWI, masuala ya uzazi na
uzazi wa mpango.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
19, Julai, 2012
No comments:
Post a Comment