Dar es Salaam.
Wanasayansi nchini Marekani wamesema kuwa wamegundua aina ya chanjo, ambayo mtu akipatiwa hataugua tena ugonjwa wa malaria maisha yake yote.
Ugunduzi huo ambao tayari umefanyiwa majaribio kwa
watu kadhaa na kufanya kazi kikamilifu ukiwa pia salama, utaandika
historia ya kufuta malaria na kuwa ugonjwa wa nadra kwa watu kuugua.
Taarifa iliyotolewa Alhamisi wiki
hii na Taasisi ya Marekani ya Kudhibiti Magonjwa ya Kuambukiza na Mzio
(NIAID), inaeleza kuwa chanjo hiyo iliyopewa jina, PfSPZ imeonyesha
mafanikio hayo kwenye hatua yake ya awali ya majaribio.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mtu akipatiwa chanjo
hiyo mwili wake unatengeneza chembe kinga ambazo zinakuwa na uwezo wa
kuangamiza vimelea wa malaria katika hatua yake ya mwanzo mara baada ya
kuumwa na mbu.
Chanjo ya PfSPZ, inaelezewa kutengenezwa kwa vimelea dhaifu wa malaria ambao huhamasisha mwili kutengeneza askari wa kudumu.
Kumbukumbu za Shirika la Afya Duniani (WHO) za
mwaka 2010, zinaonyesha kuwa zaidi ya watu 3.3 bilioni, ambao ni karibu
sawa na nusu ya dunia nzima wapo kwenye hatari ya kuugua ugonjwa wa
malaria.
Katika kipindi cha mwaka huo, inaripotiwa kuwa
watu 210 milioni walibaini kuugua malaria, baada ya kupimwa hospitalini
ambapo takriban 660,000 walipoteza maisha.
Asilimia 90 ya waliopoteza maisha walikuwa kutoka
Bara la Afrika, licha ya juhudi kubwa za kusambaza vyandarua vyenye dawa
na dawa za tiba.
WHO inasema kuwa kuongezeka kwa mbinu za kuzuia na
kutibu malaria katika maeneo mbalimbali duniani kumesaidia kupunguza
tatizo la malaria kwa asilimia 25 na kwa asilimia 33 katika Bara la
Afrika.
Imesema kuwa nchi nyingi za Afrika zina uwezo
mdogo wa kifedha, hivyo hutegemea mataifa tajiri kuzisaidia kwa
kuwezesha kupatikana vifaa vya kuzuia malaria na dawa za tiba za bei
nafuu, hata kutolewa bure kwa watoto na wajawazito.
No comments:
Post a Comment