JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA AFYA NA USTAWI WA JAMII
TAARIFA KWA UMMA KUHUSU USALAMA WA MAFUTA YATOKANAYO
NA MBEGU ZA UBUYU
- Hivi karibuni kumekuwa na ongezeko kubwa la matumizi ya mafuta yanayotokana na mbegu za ubuyu kama chakula au dawa kutokana na madai ya kuwepo manufaa ya kiafya yanayotokana na mafuta hayo.
- Mnamo tarehe 10 Julai 2013, Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) ilitoa taarifa kwa umma juu ya usalama wa mafuta yanayotokana na mbegu za ubuyu. Hata hivyo, taarifa hiyo ilipokelewa kwa mitizamo tofauti miongoni mwa jamii, watalaam na wanasayansi pamoja na vyombo vya habari na kusababisha kutolewa kwa taarifa na matamko yaliyotofautina na tamko la TFDA juu ya usalama wa mafuta hayo.
- Mafuta hayo yana kiwango kikubwa cha tindikali za mafuta ziitwazo “Cyclopropenoic fatty acids (CPFA)” ambazo huweza kusababisha athari ya kiafya endapo mafuta hayo yatatumika bila kusafishwa.
- Hakuna viwango vya kitaifa au kimataifa vya mafuta ya ubuyu ambavyo vingetumika kama vigezo vya kuamua kuhusu usalama na ubora wa mafuta hayo kwa matumizi ya binadamu. Vilevile hakuna teknolojia hapa nchini inayotumika katika kusindika mafuta hayo yenye uwezo wa kuondoa tindikali hiyo.
- Tafiti zilizofanywa kwa wanyama sehemu mbalimbali duniani, zinaonesha kuwepo athari mbalimbali za kiafya ikiwa ni pamoja na kupungua kwa ukuaji wa panya mpaka kufikia asilimia 50%, kupungua kwa utagaji wa kuku wa mayai na athari kwenye figo. Kuwepo kwa athari kwa wanyama kunaonesha uwezekano wa kuwa na madhara kwa afya ya binadamu endapo atatumia mafuta yenye tindikali ya mafuta hiyo. Aidha, athari nyingine zinazoweza kutokana na matumizi ya mafuta ya ubuyu yenye tindikali ya CPFA ni pamoja na kuathiri vimeng’enyo (enzymes) vinavyosaidia katika uchakataji wa tindikali za mafuta mwilini (fatty acid biosynthesis) hivyo kusababisha ukondefu. Taarifa zaidi za kisayansi zinaonesha kuwa matumizi ya mafuta yenye kiwango kikubwa cha CPFA sanjari na matumizi ya vyakula vilivyochafuliwa na sumu kuvu aina ya aflatoxin B1 ambayo inazalishwa na ukungu (fungus) katika baadhi ya vyakula kama vile mahindi na karanga huongeza uwezekano wa kupata saratani ya ini.
- Mnamo tarehe 31 Julai, 2013, kilifanyika kikao cha watalaamu kutoka taasisi mbalimbali ambao ni wadau katika masuala ya usalama wa chakula, utafiti, sayansi na teknolojia ili kujadili usalama wa matumizi ya ubuyu. Taasisi hizo ni Kitengo cha Tiba Asili na Mbadala, Idara ya Kinga na Mfamasia Mkuu wa Wizara (Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii),Taasisi ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Taasisi ya Tiba Asili Muhimbili, COSTEC, Shirika la Viwango (TBS), SIDO, Safe food Assurance Ltd pamoja na TFDA yenyewe.
- Pamoja na mambo mengine, wataalamu hao walikubaliana kuwa mafuta ya ubuyu ambayo hayajasafishwa kwa teknolojia inayoondoa tindikali za CPFA si salama kwa matumizi ya binadamu na yanaweza kutumika kama mali ghafi katika viwanda vinavyoweza kusafisha mafuta hayo. Aidha, teknolojia za usafishaji wa mafuta hayo zinatumika sehemu nyingine duniani na zinaweza kusafisha tindikali hiyo ya mafuta.
- Kwa kuzingatia maelezo yaliyotolewa hapo juu, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii inapenda kusisitiza mambo yafuatayo: -
- Kwamba Wizara inaitahadharisha jamii kujiepusha na matumizi ya mafuta ya mbegu za ubuyu yaliyo na tindikali za cyclopropenoic fatty acids kwa kuwa si salama kwa matumizi kama chakula au dawa.
- Ili kuepusha mkanganyiko kwa jamii kutokana na kujitokeza kwa vyanzo vingi vya taarifa zinazohusu usalama wa chakula, dawa, vipodozi na vifaa tiba, Wizara inasisitiza kuwa taasisi pekee yenye dhamana ya kutoa taarifa kwa umma juu ya usalama wa bidhaa hizo hapa nchini ni Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) pekee kama ilivyoainishwa katika Sheria ya Chakula, Dawa na Vipodozi, Sura 219.
- Wizara inatoa wito kwa wafanyabiashara na wananchi kuhakikisha kwamba bidhaa zote za chakula, dawa, vipodozi na vifaa tiba zimesajiliwa na TFDA kabla ya kusambazwa na kutumika hapa nchini na wale watakaokiuka masharti hayo watachukuliwa hatua kwa mujibu wa Sheria.
Imetolewa na
MHE. DKT. HUSSEIN A. MWINYI (MB)
WAZIRI WA AFYA NA USTAWI WA JAMII
7 AGOSTI 2013