Wednesday, December 19, 2012

WIZARA YA AFYA KUANZISHA KINGA YA KUZUIA VIFO KWA WATOTO UMRI CHINI YA MIAKA 5



WIZARA ya Afya na Ustawi wa Jamii inatarajia mwaka ujao kuanzisha chanjo mpya mbili za Pneumococcal na Rotavirus, ambazo ni maalum katika kukinga maradhi na vifo kwa watoto waliochini ya umri wa miaka mitano.

Kauli hiyo ilitolewa jijini Dar es Salaam leo, na Mkurugenzi wa Kinga, Elias Chinamo, wakati wa warsha ya siku moja ya wandishi wa habari, ya kuwajengea uwezo wa kufikisha elimu sahihi kwa jamii pamoja na kuihamasisha jamii kuhusu chanjo hizo mpya,  zitakapoanza mwaka 2013.
Alisema walengwa wa chanjo hizo watakuwa ni watoto waliyo n aumri wa chini ya miezi 12 ambapo chanjo ya kukinga nimonia (pcv13), itatolewa mara tatu kuanzia umri wa wiki sita, 10 na 14.

Chinamo alibainisha kuwa chanjo ya kinga ya kuhara  (rotavirus), itatolewa mara mbili kuanzia umri wa wiki sita na 10, inasisitizwa kuwa ili mtoto apate kinga kamili ni lazima akamilishe ratiba mapema.

Alisema kitaalam zinaonesha kuwa chanjo ya ‘Pneumococcal’ hukinga maambukizi ya nimonia kwa asilimia 38, homa ya uti wa mgongo kwa takriban asilimia 87; na chanjo ya ‘rotavirus’ hukinga  kuharisha kunakosababisha vifo vya watoto kwa aslimia 80.

Chinamo aliongeza kuwa  kwa sehemu kubwa hukinga ugonjwa wa kuharisha unaosababshwa na vimelea vya aina nyingine pia.

Alibainisha kuwa vimelea ‘Streptococcus Pneumoniae’ ni kisababishi kikuu cha maradhi na vifo vitokanavyo na ugonjwa wa nimonia na homa ya uti wa mgongo kwa watoto katika nchi zinazoendelea.

Aidha, vimelea vya ‘rotavurus’ kwa upande mwingine husababisha takriban asilimia 80 ya maradhi na vifo vitokanavyo na kuharisha kwa watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano duniani

Vile vile alitoa wito kwa wananchi kuwa chanjo hizo ni salama na zitatolewa bure bila malipo ambapo pia aliwahakikishia wananchi hao kuwa  chanjo zitatolewa na wataalam wenye uzoefu.


No comments:

Post a Comment