WIZARA
ya Afya na Ustawi wa Jamii inatarajia mwaka ujao kuanzisha chanjo mpya mbili za
Pneumococcal na Rotavirus, ambazo ni maalum katika kukinga maradhi na vifo kwa
watoto waliochini ya umri wa miaka mitano.
Kauli hiyo ilitolewa jijini Dar es Salaam leo, na Mkurugenzi wa Kinga,
Elias Chinamo, wakati wa warsha ya siku moja ya wandishi wa habari, ya
kuwajengea uwezo wa kufikisha elimu sahihi kwa jamii pamoja na kuihamasisha
jamii kuhusu chanjo hizo mpya, zitakapoanza mwaka 2013.
Alisema walengwa wa chanjo hizo watakuwa ni watoto
waliyo n aumri wa chini ya miezi 12 ambapo chanjo ya kukinga nimonia (pcv13),
itatolewa mara tatu kuanzia umri wa wiki sita, 10 na 14.
Chinamo alibainisha kuwa chanjo ya kinga ya kuhara
(rotavirus), itatolewa mara mbili kuanzia umri wa wiki sita na 10, inasisitizwa
kuwa ili mtoto apate kinga kamili ni lazima akamilishe ratiba mapema.
Alisema kitaalam zinaonesha kuwa chanjo ya
‘Pneumococcal’ hukinga maambukizi ya nimonia kwa asilimia 38, homa ya uti wa
mgongo kwa takriban asilimia 87; na chanjo ya ‘rotavirus’ hukinga kuharisha kunakosababisha vifo vya watoto kwa
aslimia 80.
Chinamo aliongeza kuwa kwa sehemu kubwa
hukinga ugonjwa wa kuharisha unaosababshwa na vimelea vya aina nyingine pia.
Alibainisha kuwa vimelea ‘Streptococcus Pneumoniae’
ni kisababishi kikuu cha maradhi na vifo vitokanavyo na ugonjwa wa nimonia na
homa ya uti wa mgongo kwa watoto katika nchi zinazoendelea.
Aidha, vimelea vya ‘rotavurus’ kwa upande mwingine
husababisha takriban asilimia 80 ya maradhi na vifo vitokanavyo na kuharisha
kwa watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano duniani
Vile vile alitoa wito kwa wananchi kuwa chanjo hizo
ni salama na zitatolewa bure bila malipo ambapo pia aliwahakikishia wananchi
hao kuwa chanjo zitatolewa na wataalam wenye uzoefu.