Friday, November 9, 2012

WATANZANIA WATAKIWA KUPIMA AFYA ZAO MARA KWA MARA-MAMA SALMA KIKWETE.


Mke wa Rais Mama Salma Kikwete (pichani) ameitaka jamii kujenga mazoea ya kujichunguza afya zao mara kwa mara ili kuepuka maradhi au vifo visivyo na lazima kwani hivi sasa kuna maradhi mbalimbali yanayotokana na mazingira na aina ya mtindo wa maisha na hivyo kurudisha nyuma maendeleo binafsi na taifa kwa ujumla.

Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) ameyasema hayo jana wakati wa uzinduzi wa kampeni ya utoaji huduma ya afya kwa jamii ikiwemo uchunguzi wa saratani iliyoandaliwa na Chama cha Madaktari Wanawake Tanzania (MEWATA) katika viwanja vya mnazi mmoja jijini Dar es Salam.

Mama Kikwete pia aliitaka jamii kubadilisha mtazamo juu ya afya ya uzazi na mtoto kuwa inamhusu mama peke yake bali kila mmoja katika familia anahusika ingawa hapo awali wanaume walionekana kutengwa na kutowajibika ipasavyo hivyo kusababisha kuzorota kwa afya ya uzazi na mtoto.

“Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii pamoja na wadau wake hivi sasa wametuanzishia mchakato huu, awali huduma hii ilijulikana kama afya ya mama na mtoto lakini sasa inajulikana kama afya ya uzazi na mtoto hii ni kuonesha kwamba kila mmoja wetu ndani ya familia anawajibika”, alisema Mama Kikwete.

Mwenyekiti huyo wa WAMA pia aliipongeza MEWATA kwa kuikumbuka jamii na kujitoa kwao kama madaktari wanawake kuweza kuwafikia wananchi wengi kwa mara moja hii inathibitisha kuwa wanawake wakipewa nafasi ya kuongoza wanaweza.

Aidha Mama Kikwete alivitaka vyombo vya habari kutia mkazo katika kuandika habari zinazohusu afya ya uzazi na mtoto kwa kuziandika habari hizo katika kurasa za mbele za gazeti na siyo katika kurasa za ndani kwani kupitia kwao jamii inapata elimu kuhusiana na mambo ya afya.

Kwa upande wake mwenyekiti wa MEWATA Dk. Serafina Mkuwa alisema kuwa tangu chama hicho kimeanza kufanya zoezi la uchunguzi wa saratani ya mlango wa kizazi mwaka 2005 hadi mwezi Machi mwaka huu wameweza kuchunguza akinamama zaidi ya elfu 65 ambapo miongoni mwao 3139 sawa na asilimai tano walikutwa na matatizo mbalimbali ya matiti na 167 sawa na asilimia 0.3 waligundulika kuwa na saratani ya matiti.

“Kwa takwimu hizi ni dhahiri kuwa kuna matatizo makubwa ndani ya jamii yetu kwa hiyo ipo haja ya kufanya jitihada za makusudi kuelimisha jamii ili iweze kujiwekea utaratibu wa upimaji afya mara kwa mara kwani matatizo ya kiafya ikiwemo saratani yakigundulika mapema na kutibiwa hupona na hivi kuboresha afya na kuleta maendeleo ya nchi”, alisema Dk.Mkuwa.

Aliendelea kusema kuwa wakati wa kampeni za uchunguzi wa saratani ya mlango wa kizazi imekuwa ngumu kwa kiasi fulani kwani wanahitaji vifaa tiba zaidi ili waweze kutibu dalili ashiria za saratani ya mlango wa uzazi ambazo mara nyingi ni rahisi kuchunguzwa katika vituo vya afya na muhudumu aliyepata mafunzo ya huduma hiyo.

Chama hicho kinategemea kufanya mkutano wake wa 13 wa mwaka wa kisayansi tarehe 10 mwezi huu jijini Dar es Salaam ambapo kauli mbiu ni Ushiriki wa wanaume katika kuboresha afya ya uzazi wa mtoto katika Afrika; je tuko wapi?

Moja ya vitu wanavyovifanya kabla ya kuanza kwa mkutano huo ni kutoa huduma za afya bure kwa siku moja ikiwemo upimaji wa afya ya mwili na kinywa kwa jamii yote ili iweze kupata huduma kutoka kwa madaktari bingwa ili wananchi wasio na uwezo wa kuonana na madaktari hao katika hospitali waweze kunufaika na huduma hiyo.





No comments:

Post a Comment