Saturday, April 14, 2012

MAMA SALMA KIKWETE AZINDUA KAMPENI YA KITAIFA YA UHAMASISHAJI WA UCHANGIAJI DAMU KUOKOA MAISHA YA MAMA WAJAWAZITO WANAOHITAJI DAMU.


Dkt. Telesphory Tryphone Kyaruzi Mkurugenzi Mtendaji wa THPI akipeana mikono na Mgeni Rasmi Mama Salma Kikwete Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) mara baada ya kutoa hotuba yake ya utangulizi. Katikati ni Naibu Waziri Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Mh. Dkt. Fenella Mukangara (MB).



Katika hotuba yake ya utangulizi Dkt. Telesphory Kyaruzi, alianza kwa kumshukuru Mgeni Rasmi Mama Sama Kikwete kwa kukubali kuwa Mgeni Rasmi katika kampeni hii ya Kitaifa ya kuchangia damu. Alisema kampeni kuu ya Saidia Mama Mjamzito ajifungue Salama inalenga kuhamasisha Taifa juu ya kutekeleza malengo ya milenia namba 4 na 5 ya kupunguza vifo vya mama na mtoto kwa asilimia 75 ifikapo mwaka 2015. Alisema swala lakuchangia damu ni swala ambalo liko katika uwezo wetu sisi watanzania. Alisema pia kwamba hiyo ni awamu ya kwanza ya kampeni hiyo ambayo kampeni itaendelea mikoani ikiwamo Shinyanga, Kigoma, Mbeya na hatimaye Tanzania nzima.



Nae Naibu Waziri Wizara Ya Habari Vijana, Utamaduni na Michezo, Mh. Dkt. Fenella Mukangara (MB), alimshukuru Mama Salma Kikwete na kumpongez a kwa kujali changamoto zinazowakabili wakina Mama na Watoto na kushiriki katika kutatua changamoto hizo. Pia aliwashukuru na kuwapongeza madaktari Vijana kupitia umoja wao wa THPI kwa kubuni na kuanzisha kampeni hiyo. Pia wizara yake ambayo ina dhamana na mambo ya Vijana, imechukulia hatua hiyo ni muendelezo wa sera ya Maendeleo ya vijana ya mwaka 2007 ambayo inaendelea kutumika hadi sasa. Pia alisema kwamba Wizara inawahimiza kuendelea kuthubutu na kupenda kazi na kujituma kwa kuzingatia sheria na malengo chanya ya kujenga Taifa letu la Tanzania. Wizara inahimiza Vijana kutumia fursa kwa kutumia weledi na utaalam wao katika Maendeleo ya Taifa. Amefurahishwa sana jinsi Vijana madaktari wameweza kutumia utaalam wao kwa kutatua kero ambayo wamekutana nayo katika sehemu yao ya kazi. Aliendelea kusema kwamba mpango unalenga katika kuhamasisha Taifa kuchangia damu ili kuweza kumaliza vifo vya kina mama na watoto. Alichukua fursa hiyo kuwataka Vijana walio kaitka taaluma mbali mbali (Youth Profesionals) kote nchini Tanzania kuweza kujiunga katika kutoa huduma mbali mbali kwa jamii kulingana na taaluma zao.



Nae Mgeni rasmi Mama Salma Kikwete katika hotuba yake alianza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutuwezesha kukutana katika uzinduzi wa Kitaifa wa kampeni ya kuchangia damu, shughuli ambayo ni muhimu kwa ustawi wa Taifa letu la Tanzania. Pia aliendelea kwa kuwapongeza madaktari Vijana wa THPI kwa kusema kwamba jambo waliliolifanya ni kubwa sana Kitaifa, la kukusanya damu kwa ajili ya kuokoa maisha ya kina mama na watoto wanaohitaji damu. Aliwataka madaktari Vijana wa THPI kuendelea kuwa na moyo huo huo bila kujali changa moto zinazowakabili, na aliahidi kuendelea kuwaunga mkono katika jitihada zao kadri muda utakavyo mruhusu. Mama Salma Kikwete alisema kuwa ifikapo mwaka 2015 lazima tuhakikishe kwamba tumefikia malengo ya MDG 4 na 5 ya kuboresha Afya ya Mtoto na kupunguza vifo vya kina mama. Alisema Tanzania imepiga hatua kubwa kwa kupunguza vifo vya watoto kutoka 578 kati ya vizazi hai 100,000 mpaka kufikia 454 kati ya vizazi hai 100,000 kutokana na juhudi kubwa zilizofanywa na serikali kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa kushirikiana na taasisi mbali mbali ikiwemo THPI. Alisema kwamba ifikapo mwaka 2015 Tanzania itafikia malengo ya milenia kwa kupunguza vifo vya kina mama na watoto mpaka kufikia 225 kwa vizazi hai 100,000. Alimaliza kwa kuwataka Vijana wote wa Tanzania kuonyesha moyo wa uzalendo kwa Taifa letu. Pia alitoa shukurani zake za dhati kwa ofisi ya Waziri Mkuu Uwekezaji na Uwezeshaji chini ya Mh. Dkt. Mary Nagu (MB), kwa Naibu Waziri Wizara ya Habari, Vijana Utamaduni na Michezo, Mh. Dkt. Fenella E. Mukangara (MB), na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii chini ya Dkt. Hadji Mponda (MB) kwa kuwawezesha Vijana madaktari kutekeleza shughuli mbali mbali ikiwemo kampeni hii. Pia Aliwapongeza wakina mama na kina baba na wananchi wote waliohudhuria katika kampeni hiyo wakiwemo wanafunzi wa Shule za Sekondari mbali mbali.



“VIJANA TUSONGE MBELEE, HATUWEZI KURUDI NYUMAA * 2,
SONGAA, SONGA MBELEE, HATUWEZI KURUDII NYUMA * 2”



Katibu Mkuu Wa THPI Dkt. Elisia Mpango katika kutoa shukrani kwa niaba ya THPI kwenye kuhitimisha kampeni hiyo alitoa shukrani zake za dhati kwa Mgeni rasmi mama Salma Kikwete kwa kukubali kushirki na kuzindua rasmi kampeni hiyo, pia alitoa shukrani kwa Naibu Waziri Wizara ya Habari, Vijana Utamaduni na Michezo Dkt. Fenella Mukangara (MB) , Mstahiki Meya wa Kinondoni Mh. Yusuph Mwenda, Katibu Tawala za Mikoa Mh. Bi. Theresia Mbando, Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii iliyowakilishwa na Dkt. Donan Mbando na wadau wote walioshiriki katika kukamilisha kampeni hiyo bila kuwasahau wakina mama, wakina baba, Vijana na wanafunzi wa sekondari na wote walioshiriki na kukubali kuchangia damu kwa hiari yao. Alisema katika kampeni hiyo jumla ya chupa 150 za damu zilikusanywa. Aliwaasa wahisani mbali mbali wajitokeze katika awamu zinazofuata za kampeni hiyo ili kuwezesha mwendelezo wa kampeni ya SAIDIA MAMA MJAMZITO AJIFUNGUE SALAMA.




Friday, April 6, 2012

THPI YAANZISHA KAMPENI YA KITAIFA YA KUCHANGIA DAMU ILIYOZINDULIWA NA MAMA SALMA KIKWETE


Mkurugenzi mtendaji wa THPI Dr. Telesphory Kyaruzi akitoa historia fupi ya taasisi hiyo pamoja na kuelezea kampeni ya "Saidia mama mjamzito ajifungue salama" kwa kuchangia damu katika awamu ya kwanza kitaifa. Wanaofuatilia kulia ni Naibu Waziri Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Mh. Dkt. Fenella E. Mukangara (MB), mgeni rasmi Mama Salma Kikwete mwenyekiti wa taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) , na katibu tawala mkoa wa Dar es Salaam Bi. Theresia Mbando.
Kampeni imelenga kukusanya damu kwa ajili ya kuwasaidia wakina mama wajawazito wanaohitaji damu kabla ya kujifungua wakati wa kujifungua na baada ya kujifungua, na wale ambao wanajifungua kwa upasuaji.

Monday, April 2, 2012

THPI YAANDAA KAMPENI YA KITAIFA YA KUCHANGISHA DAMU ILIYOZINDULIWA NA MAMA SALMA KIKWETE




Mama Salma Kikwete akiwasili katika viwanja vya Biafra Kinondoni wakati wa uzinduzi wa kampeni ya kitaifa ya kuchangisha damu iliyofanyika katika viwanja hivyo. Anaesalimiana nae ni naibu waziri wa habari, vijana, utamaduni na michezo Mh. Dkt. Fenella Mukangara (MB) na anaefuata ni meya wa kinondoni Mh. Yusuph Mwenda. Katika kampeni hiyo jumla ya unit 150 za damu zilipatikana na zitatumika kuwasaidia wakina mama wajawazito wanaohitaji damu.